PICHANI: Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi na Tiba cha St Glory, Felister Massawe akionesha barua ambayo ameandikiwa na NACTE kusimamishwa kwa chuo hicho kwa siku 14 ili kurekebisha mapungufu yaliyopo na sio kufungiwa kabisa kama watu walivyotangaza.
Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
Siku chache baada ya Baraza la kusimamia Vyuo vya Elimu ya Ufundi (NACTE) Kukifungia Chuo cha Elimu ya Tiba na Uuguzi cha St.Glory, Mkurugenzi wa Chuo hicho, Felister Massawe ajitokeza hadharani na kueleza mapungufu machache yaliyopelekea wao kupata adhabu ya kusimamishwa kwa siku 14.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Chuo Bi. Felister Massawe amesema kuwa habari zilizotangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa wamefungiwa si kweli bali NACTE wamewapa siku 14 za kurekebisha kasoro za kiutawala.
"Napenda kuwatangazia watanzania kuwa Chuo chetu hakijafungwa bali kimesimamishwa kwa siku 14 kutokana na madai kwa baadhi ya wafanyakazi wetu kupeleka taarifa NACTE kuwa wanatudai Milioni 150 kwa ajili ya mishahara jambo ambalo si la kweli hivyo kwa sasa tumeamua kushughulikia changamoto hiyo hili tuweze kuanza upya" amesema
Massawe amesema kuwa kumekuwa na wafanyakazi wa Chuo ambao wamekuwa sio waaminifu katika utumishi wao kiasi cha kuchapisha nyaraka za uongo na kuzipeleka NACTE wakidai kuwa walikuwa na mkataba wa kulipwa Milioni 9 kwa mwezi jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa chuo hiki.
Amesema kuwa mikataba ya watumishi hao ilikuwa ni laki 9 lakini wameamua kuongeza sifuri ili kuwahadaa NACTE waweze kuamini wanachokisema na kupelekea kusimamishwa kwa chuo kwa siku 14.
Awali watumishi hao walisimamishwa kazi kwa utovu wa nidhamu mara baada ya kuonekana wanachochea migomo kwa wanafunzi jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi wa taaluma ya afya kwa kupotezea umakini darasani.
Kwa upande wake wakili wa chuo hicho Zaidi Mwesigwa amesema kwa sasa atawafungulia mashtaka ya jinai kwa kufoji nyaraka wale wote ambao wamehusika kupeleka barua hizo NACTE.
Mwanasheria na Wakili wa kujitgemea wa Chuo Cha S.t Glory kilichopo Kimara jijini Dar es Salaam, Zaidi Mwesigwa akitoa maelekezo ya kisheria yatakayochukuliwa kwa watu wote waliojaribu kudanganya ili kukichafua Chuo hicho.
Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi na Tiba cha St Glory , Felister Massawe akijadiliana jambo na Mwanasheria wake Zaidi Mwesigwa pamoja na Afisa Utawala mara baada ya kumaliza kuongea na Waandishi wa habari.