Songea
Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma linamshikilia Fikiri Mapunda (32) mkazi wa kitongoji cha Msirikasi kilichopo kijiji cha Malunga kata ya Tingi wilaya ya Nyasa kwa tuhuma za kumchoma kisu shingoni Yakobo Mbungu (29) mkazi wa kitongoji hicho wakati wakinywa pombe za kienyeji ambapo alifariki muda mchache wakati akikimbizwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Mbinga kwa ajili ya matibabu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeke amesema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa nne usiku kwenye klabu za pombe za kienyeji ,ambapo Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wakinywa pombe ghafla walianza kurushiana maneno ambapo inadaiwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa mapenzi.
Amefafanua zaidi kuwa, Yakobo anadaiwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Vumi Kawonga ambaye kwa siku za nyuma kabla ajaanza kuwa na mahusiano na mapunda alikuwa ni mpenzi wa marehemu.
Ameongeza kuwa, siku ya tukio inadaiwa mapunda na Marehemu walikutana kwenye hicho klabu ambapo walianza kurushiana maneno na kila mmoja alimtuhumu mwenzake kuwa alimuibia mpenzi wake na baadaye ulizuka ugomvi mkubwa kisha Yakobo alichomwa kisu na kumwaga damu nyingi ambazo zilisababisha apoteze maisha.
Amesema, mara baada ya uongozi wa serikali ya kijiji kupata taarifa za mauaji hayo ulimkamata mtuhumiwa na kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha Mbambabay ambapo anaendelea kushikiliwa na Jeshi hilo hadi upelelezi wa polisi utakapokamilika kwa ajili ya kumpeleka mahakamani.