
PICHA: Baadhi ya Wanachama wa KIRISHI wakiingia kwenye moja ya gari liliwapeleka katika mradi wa shamba lililopo Zinga, Bagamoyo jumapili asubuhi.
Na Mwandishi Wetu, Immamtukio

Katika ziara hiyo iliyoandaliwa kwa lengo maalumu la kuonesha hatua zilizofikiwa katika mradi wa kilimo, uongozi wa KIRISHI (Kinondoni Rise and Shine Investment) ulionesha mazoa biashara matatu yaliyopandwa katika heka 4 mpaka sasa wakati shamba ni la ukubwa wa heka 10. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa KIRISHI, Bw. Efatha Masuki, mazao yaliyopandwa ni Bamia, Nyanya na Matikiti.
“Kwasasa mazao ni matatu, eneo la heka 6 lililobaki linaadaliwa kwaajili ya kuotesha mazao ya mbogamboga.” Alieleza Bw. Masuki. “Eneo hili ni mfano (Demo) kwaajili ya kuwaandaa wanachama ili kusudi wanapotaka kuendelea na kilimo wawe na mfumo unaoeleweka” aliongeza Bw. Masuki.
Naye Katibu wa Kamati ya Usimamizi na Ustawi wa KIRISHI, Bw. David Musiba, alieleza mpango wa baadae kuwa “ katika heka 4 zilizotumika, tikiti ni heka 1.45 ambapo kuna mshimo yasiyopungua 1,740, pia tuna nyanya heka 1 ambapo kuna matuta 60 yenye miche isiyopungua 30 katika kila tuta, bamia tumelima heka 1”
Bamia ambazo tayari zimeshaanza kutoa maua, ziko tayari kuvunwa na kwa kuanzia baadhi ya wanachama walipata fursa ya kununua kwa mafungu ikiwa ni mvuno wa kwanza. Hata hivyo KIRISHI imeanza maandalizi ya kilimo cha mazao kama matango, bilinganya na roshuu. Mpango wa baadae ni kuweka mboga kama mchicha, mnavu na majani ya maboga pamoja na matembele.
Mtaalamu Msimamizi wa Kilimo kutoka shirika la SAVIA, Noodin Mndoholele ameahidi kusimamia kiutalaamu na kuhakikisha malengo yanatimia kama ilivyopangwa. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema “ili kuhakikisha tunapata mazao bora tutatumia mbolea itakayoboresha utoaji wa maua na tutatumia dawa iitwayo MOP ambayo kwa mara ya kwanza inatambulishwa na kampuni ya SAVIA”
Bw. Mndoholele anasema dawa ya MOP itachanganywa kitaalamu na mbolea ya urea ili kuhakikisha utoaji wa maua na kutokupukutika kwa maua unazingatiwa ili kuboresha na kupata mazao mengi na yenye bora.
Baadhi ya wanachama walioshiriki ziara hiyo waliushukuru uongozi wa KIRISHI kwa jitihada walizoweka katika kutimiza malengo ya kikundi. Kwa kutumia mtandao wa KIRISHI wa Whatsaap Bi. Anna Shayo anaandika
“Napenda kumshukuru Mungu kwa kutufikisha shambani na kurudi salama. Niwapongeze viongozi wetu kwa kazi kubwa waliofanya. Pia sisi wenyewe tujipongeze kwa michango yetu iliyowezesha kufikisha ile kazi katika hatua ilyofikia. Mungu ni mwema tuendelee kukazana. Pia tujitahidi kusahihisha mapungufu tuliyoyaona ili tugonge pale tulipolenga. Asanteni sana wote kwa jumla. Viongozi tunawaomba msife moyo tusukume hilo gurudumu kwa pamoja. Mungu awabariki.”

Baadhi ya wanachama wakifurahia matunda

Baadhi ya wanachama wa KIRISHI wakikagua maendeleo ya shamba lao, Zinga wilayani Bagamoyo

Baadhi ya wanachama wakipata picha katikati ya shamba la bamia
Zao la Bamia likiwa tayari kuvunwa

Katibu wa Kamati ya Usimamizi na Ustawi, David Musiba (aliyeinua mikono) akitoa maelezo kwa baadhi ya wanachama kuhusiana na moja ya malambo yaliyopo shambani hapo kwaajili ya umwagiliaji


Mche wa nyanya ukisubiri maandalizi ya kuinua



Mtaalamu wa mipango akitoa maelezo kuhusu hatua zilizofikiwa za maandalizi ya mpango mkakati


Mmoja wa wanachama wa KIRISHI akichangia











