Leo Ramadhani 11
MAELEZO YA AWALI
Baada ya kumaliza kumi la kwanza ambalo ni kumi la rehema, sasa tuko katika kumi la kati ambalo ni kundi la MAGHAFIRA. Waumini wengi wameendelea kushindana na kupupia katika kufanya ibada. Pamoja na hayo, wapo waumini waliojisahau katika kufanya ibada na hasa Swala ya TARAWEHE
CHANZO CHA TARAWEHE
Swala ya Tarawehe ni Sunna maarufu, inayoswaliwa baada ya Swala ya Isha, kila siku, usiku, katika Mfungo wa Ramadhani. Na imeitwa Tarawehe, kwa sababu baada ya kila rakaa nne, watu hupumzika, kidogo, kisha kuendelea. Na ni Swala inayo swaliwa rakaa mbili mbili, kwa kupumzika kidogo, na baada ya kukamilisha rakaaa nne, basi hupumzika kwa muda zaidi.
Ni Swala ambayo, siyo tu, ameiswali Mtume mwenyewe msikitini, bali ameiswalisha jamaa, kwa muda wa siku tatu mfululizo. Na watu walikuwa wakiongezeka kuja kuswali nyuma yake, kiasi kwamba siku ya nne, msikiti haukutosha! Mtume hakutoka tena kwenda kuswali Swala hiyo, licha ya watu kunadi kuwa wakati wa Swala hiyo umewadia. Mtume hakuitikia wito wao huo. Na hakuenda msikitini, hadi alfajiri kwa ajili ya Swala ya Alfajiri.
Aliwaswalisha Alfajiri, kama kawaida. Lakini, alipomaliza, tu, aliwageukia waumini na kuwaeleza kwanini hakuenda msikitini; alichelea kwamba lau angeliendelea hivyo hivyo, na watu wakawa wanaongezeka kila siku, basi ingeliwezekana ً ikafaradhishwa Swala hiyo, juu yao. Na wasingeliweza kutimiza jukumu hilo zito. Hivyo, akaonelea bora aswali nyumbani, na hivyo Swala ya Tarawehe isalie kuwa ni Sunna kubwa sana, katika Mfungo wa Ramadhani. Na alikuwa akiwahimiza sana watu kuiswali pasi na kuwalazimisha.
Imepokewa kutoka kwa Bi. Aisha akisema: “Alitoka, Mtume usiku mmoja akaenda kuswali msikitini. Watu wakamfuata nyuma katika Swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakawa wanaambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wengi zaidi wakajumuika, siku ya pili.
Mtume akaenda tena usiku wa pili msikitini. Watu wengi zaidi wakamfuata katika swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakaanza kuambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wakajumuika kwa wingi zaidi msikitini.
Mtume akaenda tena usiku wa siku ya tatu, ambako kulikuwa na watu wengi zaidi. Akaswali siku ya tatu, na watu wakamfuata kwa swala yake hiyo.
Ulipoingia usiku wa siku ya nne, msikiti haukuweza kuwa na nafasi ya kutosha watu wote waliokwenda. Mtume hakuenda msikitini. Watu wakaanza kuita kwa kusema: “Swalaaa! Swalaaa!” Lakini Mtume hajaenda!
Ilipoingia Alfajiri ndiyo akaenda msikitini kwa Swala ya Alfajiri.
Alipomaliza kuswali Alfajiri, aliwageukia watu na kutoa Shahada, na kisha kusema: " Si kama nilikuwa sijui kuhusu kujumuika kwenu jana usiku, msikitini! Nilikuwa najua vilivyo! Ila nilichelea isije Swala hiyo ikafaradhishwa juu yenu, na halafu mkashindwa kuitekeleza" (Bukhari na Muslim).
Inasemekana Swala hiyo ilikuwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.” Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra akisema: Amesema Mtume “Atayefanya Ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani safi kabisa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huku akiwa na matarajio ya malipo ya Mwenyezi Mungu Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia” Muttafaq ‘alayhi. Pia Imepokewa, kutoka kwa Abu Hurayra akisema: “Alikuwa Mtume akiwahimiza sana watu kufanya ibada usiku wa mwezi wa Ramadhani (mzima) pasi na kuwalazimisha, kwa kusema: “Atayefanya ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani safi kabisa kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwa na matarajio ya malipo ya Mwenyezi Mungu, Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia” (Muslim)
UMUHIMU WA SWALA HII
Kutokana na maelezo hayo hapo juu, Swala ya Tarawehe ni Sunna kubwa sana, na ina fadhila kubwa sana, na Mtume ameiswali, na kuswalisha msikitini. Na baada ya kuacha kwenda kuiswalisha msikitini, watu waliendelea kuiswali katika jamaa ndogo ndogo, au kila mtu peke yake.
Imam Bukhari amepokea Hadithi kutoka kwa Ibn Shihab, kuhusu watu kuendelea kuswali Tarawehe, katika jamaa ndogo ndogo, au mtu binafsi, akisema:
“Na mtindo huo ukaendela baada ya kifo cha Mtume na enzi ya Abu Bakr na kipindi cha mwanzo cha enzi ya Umar bin al-Khattab Lakini, Umar akaona ni vyema kuwakusanya watu wote, nyuma ya Imamu mmoja. Hivyo, akamtaka Ubayy bin Ka’b aswalishe jamaa moja.
Imepokewa kutoka kwa Abdurrahman bin Abdulqaari’ akisema: “Nilifuatana usiku mmoja wa Ramadhani, na Umar bin al-Khattwab kwenda msikitini. Akaona watu wanaswali, kwa mitindo tofauti tofauti; ama wanaswali kila mmoja peke yake, au wengine wanamfuata imamu mmoja, na wengine wanamfuata imamu mwengine. Basi akasema: “Ya leti watu hawa wangekusanyika nyuma ya mtu mmoja. Ingelikuwa bora zaidi!” Hivyo, baada ya hapo akaazimia kuwakusanya waswali nyuma ya Ubayy bin Ka’b (Bukhari)
MAMBO YA KUZINGATIA
Ili Muislami apate faida katika ibada hii ambayo pia hupatikana ndani ya mwezi huu, na kwa utukufu wa mwezi huu hapaswi kupuuza pia azingatie kuwa:-
• Swala ya Tarawehe, au Swalat al-Layl, katika Ramadhani, ni Sunna Muakkadah –iliyotiliwa nguvu.
• Mtume ameswali na kuswalisha Tarawehe, msikitini, kwa muda wa siku tatu mfululizo. Na kuiswali, peke yake nyumbani.
• Mtume amehimiza Waislamu –pasi na kuwalazimisha- kuswali Tarawehe!
• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa bila ya jamaa, au jamaa zaidi ya moja.
• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa nyumbani au msikitini.
• Wakati wa Swala ya Tarawehe ni baina ya kumaliza Swala ya Isha, hadi kuchomoza alfajiri ya mwanzo.
• Kuswali Tarawehe, mara tu baada ya kumaliza Swala ya Isha na Sunna zake, ndio bora zaidi, kwa wanaotaka kuswali jamaa.
• Kuswali jamaa moja, nyuma ya Imamu mmoja ni Sunna kutoka kwa Mtume na vile vile, ni Sunna aliyeiendeleza, rasmi, Sayyidina Umar nyuma ya Sayyidina Umab bin Ka’b!
• Kuswali jamaa moja, katika msikiti mmoja, nyuma ya Imam aliyehifadhi Qur’ani, ni Sunna ilyorithiwa kutoka kwa Sayyidina Umar
• Ubayy bin Ka’b alikuwa haafidh wa Qur’ani, na msomaji mzuri zaidi, kwa sauti, naghama na kanuni, kuliko maswahaba wengine wote. Mtume amesema: “Ubayy ndiye msomaji mzuri zaidi miongoni mwenu!”
• Imamu bora wa kuongoza Swala ya Tarawehe ni aliyehifadhi Qur’ani, na mwenye sauti nzuri.
• Mwenye kusimama kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa nia safi, na kutaraji Fadhila za Mwenyezi Mungu tu hufutiwa madhambi yake yaliyopita.
• Mwenye kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa kujionesha, au kuonesha wengine kuwa yeye ni “Mwislamu” safi, hana anachokipata kutoka kwa Mwnyezi Mungu.