Quantcast
Channel: Matukio
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3497

MTO MALAGARASI KUZALISHA MEGAWATI 44 ZA UMEME

$
0
0
PICHA: Mwananchi wa Kijiji cha Malinzi, Kata ya Malinzi, Wilaya ya Kigoma, Hamza Poroto, akiuliza swali kuhusu huduma ya umeme wa REA, kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (hayupo pichani), wakati wa ziara yake kijijini hapo hivi karibuni. 

Na Veronica Simba – Kibondo

Mto Malagarasi ulioko mkoani Kigoma, unatarajiwa kuanza kuzalisha megawati 44.8 za umeme mara baada ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka ujao wa Fedha (2016/2017), kupitishwa na utekelezaji wake kuanza. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amesema uzalishaji huo wa umeme utatekelezwa kupitia mradi wa Igamba III.

Aliyasema hayo hivi karibuni mjini Kibondo akiwa katika ziara ya kazi, kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara yake, hususan inayohusu umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akifafanua zaidi kuhusu utekelezwaji wa Mradi huo, Naibu Waziri Kalemani alisema, Mtafiti aliyepewa kazi ya kutafiti kuhusu Mradi huo, aligundua kuwa, Igamba III inaweza kuzalisha umeme zaidi ya mara nne ya ule ulioainishwa awali katika utafiti wa Mradi wa Igamba II.

Alisema, umeme utakaozalishwa kupitia Igamba III, utatosheleza mahitaji kwa watumiaji wa nishati hiyo katika Mkoa wa Kigoma na kubaki ziada kubwa, hivyo kuondoa kabisa tatizo la umeme katika mkoa huo. “Kwa sasa, matumizi ya umeme kwa Mkoa wa Kigoma ni Megawati Sita kwa siku. Umeme utakaozalishwa kupitia Mto Malagarasi, utakuwa zaidi ya mara Saba ya mahitaji yenu,” alisema.

KUSHOTO: Sehemu ya Mtambo wa kuzalisha umeme wa mafuta unaomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mjini Kigoma.

Akielezea mipango ya uzalishaji umeme kwa kutumia maji ya Mto Malagarasi, Naibu Waziri alisema, mwaka 2009, wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Changamoto za Milenia (MCC), Mradi wa uzalishaji umeme wa Igamba II ulifanyiwa utafiti, ambapo ulipata ufadhili wa zaidi ya Dola Milioni 15 za Marekani.

Alisema, kwa bahati mbaya, kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, ilionekana hauwezi kutekelezeka kutokana na kugundulika kuwa kuna Vyura na Konokono katika Mto huo. “Kutokana na Sheria za Mazingira za Kimataifa, Mradi ule ukasimamishwa.”

Dk Kalemani alieleza kuwa, kufuatia kusimamishwa kwa Mradi wa uzalishaji umeme wa Igamba II, Serikali iliamua kutumia pesa zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wake, kununua Mashine za Umeme-Jua (Sola) katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine jirani. Maeneo hayo yalihusisha sehemu muhimu kama Hospitali, Shule mbalimbali na kwenye Masoko.

Alisema kuwa, sehemu nyingine ya fedha hizo, ilitumika kukarabati miundombinu ya umeme ya mkoa wa Kigoma na maeneo jirani ya Halmashauri zote, zikiwemo Transfoma na Nguzo za umeme. Aidha, aliongeza kuwa, fedha nyingine iliyosalia, ilipelekwa kutekeleza miradi mingine ya kimaendeleo ya Watanzania.

Naibu Waziri alisema, ili kuhakikisha wananchi wa Kigoma wanapata umeme wa uhakika na wa bei nafuu, Serikali iliamua kufanya utafiti mwingine wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji ya Mto Malagarasi, ambapo Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo, amekamilisha utafiti wake na kilichobaki ni utekelezaji wa Igamba III.

Naibu Waziri Kalemani, yupo katika ziara ya kazi ya siku 10, kukagua miradi inayotekelezwa chini ya Wizara yake katika Mikoa ya Tabora, Kigoma na Geita.

CAPTIONS

Umeme Kigoma


Umeme Kigoma 2










Viewing all articles
Browse latest Browse all 3497

Trending Articles